Uchanganuzi wa usemi wa kisiasa kuhusu nchi ya kenya katika blogu teule zilizoandikwa katika Kiswahili
Abstract/ Overview
Maendeleo ya kiteknolojia kimtandao yanazidi kubadilisha namna masuala ya kisiasa yanavyowasilishwa. Majilio ya kuandika habari na kutolea maoni katika blogu yameshuhudia kuongezeka kwa watu wanaozuru blogu na kuchangia kuhusu masuala ya kijamii na ya kisiasa yanayowaathiri. Njia hii ya mawasiliano imekuwa jukwaa muhimu kwa kuelezea mitazamo hususan kutoa nafasi huru isiyodhibitiwa. Sifa kuu katika blogu ni msingi wa viegemezi vyake vya kufasili ili kuelewa maswala ibuka. Hali inayosababishwa na matumizi ya lugha hasa na wanablogu wanapoeleza hisia, mitazamo na misimamo yao ambayo huweza kuaminika au kuwa imetiwa chumvi, kupotosha na kuchochea. Jambo hili linazua haja ya kuchunguza namna wanablogu wanavyotumia lugha wanapojadili maswala ya kisiasa nchini Kenya. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchanganua kiuhakikifu usemi wa kisiasa nchini Kenya katika blogu teule zilizoandikwa kwa Kiswahili. Madhumuni mahsusi yalikuwa ni: kubainisha na kueleza misingi inayochangia uzalishaji wa usemi kuhusu siasa katika blogu zilizoandikwa kwa Kiswahili; kudadavua maumbo ya lugha ambayo husimba tafkira za wanablogu wanapojadili maswala ya kisiasa nchini Kenya; kuchanganua mitindo mbalimbali ya lugha inayotumiwa na wanablogu wanapojadili maswala ya kisiasa nchini Kenya. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Uhakiki Changanuzi wa Usemi kama ilivyofafanuliwa na Fairclough (1997) na nadharia ya Rejista ya Halliday (1978). Muundo wa utafiti ulioshirikishwa ni wa kichanganuzi. Ili kuyafikia malengo, utafiti huu ulijikita katika blogu nne zilizoandikwa kwa Kiswahili na ambazo zilijadili maswala ya kisiasa nchini Kenya. Maswala ya kisiasa yaliyorejelewa ni katika kipindi cha mwaka wa 2008 hadi 2012 kilichoshuhudia mivutano ya kisiasa kati ya vyama viwili vikuu wakati huo; PNU na ODM na vilivyounda serikali ya mseto. Sampuli dhamirifu ilitumika kuteua blogu hizo kwa sababu zilikuwa na habari zilizohitajika katika utafiti huu. Sampuli dabwadabwa ilitumiwa kuteua matini zilizoandikwa kwa Kiswahili kuhusu maswala ya kisiasa katika blogu. Orodha ya uchunzaji, yenye misingi iliyoibua usemi, maumbo ya lugha na mitindo ya lugha ilitumiwa kukusanya na kupanga data. Data ilikusanywa na kuchanganuliwa kithamani. Misingi iliyoibua usemi, maumbo ya lugha na mitindo ya lugha ilibainishwa na kuelezwa ilivyodhihirika. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa misingi iliyochangia kuibua usemi katika blogu ni pamoja na mikakati ya urejelezi, uarifishaji na kutoa hoja. Ilibainika kuwa wanablogu hutumia maumbo ya lugha kama vile ruwaza za uelekezi, uchukulio na usonde kudumisha tafkira zao wanapojadili maswala ya kisiasa kusisitiza sifa mbaya za serikali.Yamkini, mitindo ya lugha kama vile matumizi ya lugha ya mafumbo na lugha isiyo ya kikongamano yalibainika katika usemi. Utafiti huu ulichangia kwa ujumla, katika kuonyesha umuhimu wa Kiswahili kama lugha inayotumika na wanablogu kujadili masuala ya kisiasa katika blogu kwa kushirikisha mitazamo tofauti tofauti.